
Chama cha mtandao wa Wanamuziki hapa Tanzania, kinatarajia kufanya kampeni kabambe ya kupambana na wizi wa kazi za Wasanii uliokithiri kwa kiasi kikubwa.
Rais wa chama hicho na mwanamuziki wa bendi ya The Kilimanjaro Band ‘Wananjenje’, John Kitime alieleza kuwa kampeni hiyo itaambatana pamoja na uzinduzi wa nembo mpya (inayoitwa HAKIGRAM) itakayotumika kuzuia uharamia huo unaofanywa na baadhi ya Watu wachache kwa manufaa yao binafsi.
“tunatarajia kufanya kampeni kubwa sana ya kuielimisha jamii pamoja na kuitangaza nembo hiyo mpya ambayo itawekwa kwenye kanda za kaseti,Video,VCD,DVD,ambayo itasaidia kuzuia uharamia huo,
nembo hiyo itatolewa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari yakiwemo magazeti, redio,na televisheni. Yote hiyo ni kutaka kuleta muamko ndani ya jamii, itambue kuwa kuna kitu cha namna hiyo wanapaswa kukifahamu”,alieleza Rais Kitime.
Changamoto hiyo pia itakuwa ni kwa Wafanyabiashara wote wa kazi hizo, kuhakikisha kuwa wanauza kazi za Wasanii zikiwa tayari na nembo hiyo, kinyume cha hapo watakuwa wamekiuka na watachukuliwa hatua za kisheria juu ya masuala ya hakimiliki.
“Wafanyabiashara watapaswa kuweka alama hiyo katika kazi za wasanii watakazokuwa wanaziuza, kutokuweka alama hiyo litakuwa ni kosa la jinai, hivyo kifungu cha sheria ya masuala ya hakimiliki kitatumika, ambapo muhusika akibainika atalipa faini ama kifungo”,alifafanua zaidi raisi huyo.
Aidha rais Kitime alimaliza kwa kueleza kuwa katika kampeni hiyo nembo hiyo itaonyeshwa ilivyo, itaelezwa ni namna gani itawasaidia Wafanyabiashara, wasanii,wanajamii halikadhalika na Serikali katika suala zima la ukusanyaji kodi.